Aliyekua kiungo wa klabu bingwa nchini Italia Juventus FC Claudio Marchisio amejiunga na klabu ya Zenit St Petersburg ya Urusi, kwa mkataba wa miaka mitano.
Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 32 amejiunga na klabu hiyo akiwa mchezaji huru, baada ya uongozi wa Juventus kuvunja mkataba wake mwanzoni mwa mwezi uliopita, kufuatia tatizo la kukaa nje kwa muda mrefu, baada ya kuwa majeruhi.
Kabla ya kukamilisha mpango wa kujiunga na Zenit St Petersburg, Marchisio, alikua anahusishwa na taarifa za kuwaniwa na Paris Saint-Germain, AS Monaco, Nice (Ufaransa), FC Porto, SL Benfica (Ureno) na klabu ya Montreal Impact inayoshiriki ligi ya nchini Marekani (MLS).
Marchisio ataanza maisha mapya ya soka lake nchini Urusi, baada ya kupona majeraha ya goti yaliyokua yakimsumbua kwa muda mrefu, na tayari baadhi ya vyombo vya habari vimeanza kuihusisha safari ya kuelekea nchini humo na makocha Luciano Spalletti na Roberto Mancini, ambao waliwahi kufanya kazi kwenye klabu ya Zenit St Petersburg.
Wawili hao wanatajwa kumshawishi Marchisio kujiunga na klabu hiyo na kuzikacha klabu nyingine zilizokua na lengo la kumsajili, huku wakiamini atakapokua Urusi atapata nafasi ya kucheza soka lake kwa uhuru na amani.
Luciano Spalletti alikinoa kikosi cha Zenit St Petersburg kuanzia mwaka 2009 hadi 2014, na Roberto Mancini alitua klabuni hapo kuanzia mwaka 2017 hadi 2018.