Viungo watatu wa Simba SC, Sadio Kanoute, Fabrice Ngoma na Mzamiru Yassin wamemwagiwa sifa na Kocha Mkuu wa timu hiyo, Abdelhak Benchikha.
Kama ambavyo kocha aliyepita wa Simba SC, Oliveira Roberto ‘Robertinho’ alipotua hapa nchini na kumpa sifa Mshambuliaji Kibu Denis, ndivyo hivyo ambavyo Benchikha amefanya kwa mastaa hao.
Benchikha ameweka wazi kwamba viungo wake wanafanya kazi nzuri katika kuhakikisha kwamba wanakaba, lakini pia wanapiga pasi za uhakika kwenda mbele na wameonyesha jinsi gani wanataka kuona timu hiyo inapata ushindi.
Kocha huyo raia wa Algeria amesema hana wasiwasi na kazi inayofanywa na wachezaji wengine, lakini inabidi waendelee kupambana na kurekebisha makosa madogo madogo.
“Viungo wangu Kanoute, Ngoma na Mzamiru wanafanya kazi nzuri sana, wanachukua mipira kwa wapinzani lakini pia ni wepesi katika kupeleka mashambulizi ukweli navutiwa na kazi wanayoifanya,” amesema.
“Eneo la ushambuliaji kuna changamoto kidogo kwa sababu hatujafunga mabao mengi, ila nafanyia kazi hali hiyo na naamini baada ya muda kila kitu kitakaa sawa.”
Kocha huyo ambaye alikuwa akiwania tuzo ya kocha bora wa Afrika, amesema mchezo ujao wa makundi dhidi ya Wydad Casablanca wanahitaji ushindi ili kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kufuzu Robo Fainali.
“Hakuna kitu kingine kinachohitajika kwenye mchezo na Wydad zaidi ya pointi tatu. Hii ni sawa na Fainali kwetu kwa sababu tukishinda tutakuwa na pointi tano ambazo zinaweza kutupa matumaini ya kufuzu kwenda Robo Fainali. Mashabiki wajitokeze kuisapoti timu kwa kuwa wamekuwa watu muhimu sana kwetu.”
Benchikha alianza kuwashuhuhudia viungo hao akiwa hajaanza kuinoa Simba SC kwenye mchezo dhidi ya Asec Mimosas ambao ulichezwa kwenye Uwanja wa Mkapa na kumalizika kwa sare 1-1.
Katika mnchezo huo kwenye eneo la kiungo walianza Fabrice Ngoma na Mzamiru Yassin na baadae alitoka Ngoma na kuingia Kanoute.