Mchezaji bora wa soka barani Asia Abdelkarim Hassan, amefungiwa kucheza soka kwa muda wa miezi mitano, kufuatia utovu wa nidhamu aliouonyesha dhidi ya mwamuzi aliyechezesha mchezo wa nusu fainali ya ligi ya mabinbwa barani humo Oktoba Mosi.
Beki huyo wa klabu ya Al Sadd ya nchini Qatar, alionyesha utovu wa nidhamu walipokutana na Al Hilal ya Saudi Arabia, na kupelekea adhabu ya kuonyeshwa kadi nyekundu, ambayo hakuiridhia na kujikuta akilumbana na mwamuzi hadi kutaka kuzichapa.
Shirikisho la soka barani Asia (AFC) limetoa taarifa ya kumfungia Abdelkarim Hassan, anaecheza nafasi ya beki wa kushoto, na anatarajiwa kurejea tena uwanjani Machi 20.
Abdelkarim Hassan wa kwanza kushoto akizuiwa ili asiendelee kuonyesha utovu wa nidhamu kwa mwamuzi, baada ya kupewa adhabu ya kadi nyekundu.
Hata hivyo shirikisho la soka duniani FIFA limeingilia kati adhabu hiyo na kutengua baadhi ya maagizo ya adhabu hiyo, kwa kumuwezesha Abdelkarim kucheza michuano ya klabu bingwa duniani mwezi Disemba, pia ataweza kucheza michezo ya ligi ya Qatar.
Kwa mantiki hiyo beki huyo mwenye umri wa miaka 26, ataendelea kutumikia kifungo chake upande wa michuano ya ligi ya mabingwa barani Asia.