Wakati Tanzania ikiendelea kutoa kipaumbele kwa Wachezaji wa Kigeni hasa wanapofanya vizuri katika Klabu walizosajiliwa, Beki wa zamani wa klabu za Simba SC na Coastal Union Abdul Banda amesema kasumba hiyo ni tofauti katika soka la Afrika Kusini.
Banda ambaye msimu uliopita aliitumikia Mtibwa Sugar kabla kurejea tena Afrika Kusini kujiunga na Chipa United, amesema Soka la nchini humo lina tofauti kubwa sana na Tanzania.
Amesema yeye ni mchezaji wa Kigeni katika Ligi Kuu ya Afrika Kusini, lakini anachukuliwa kawaida kutokana na wenyeji kuamini kiwango chake kwanza na mambo mengine yanafuata.
“Huku ‘maproo’ tunatuchukulia kawaida sana hakuna tofauti na wazawa ingawa hiyo ni kengele kwa mgeni kufanya kazi ili kuendelea kusalia katika timu, ila ukitukuta mazoezini ama ninapokaa huwezi ona tofaut yoyote.”
“Wanachotaka ni kazi na siyo kunyenyekewa nje ya uwanja, tofauti na Tanzania ambako mgeni anapewa thamani kubwa zaidi ya mzawa” amesema Banda
Awali Abdi Banda aliondoka Tanzania mwaka 2017 na kutimkia Afrika Kusini, ambako alisajiliwa na Klabu ya Baroka FC (2017–2019) na baadae alijiunga na Highlands Park (2019–2020) kabla ya kurejea Ligi Kuu Tanzania Bara kuitumikia Mtibwa Sugarmsimu uliopita.