Abiria 47 waliokuwa wakisafiri kutoka Mkoa wa Arusha kwenda Dar es Salaam nchini Tanzania wamenusurika kifo baada ya basi walilokuwa wakisafiria mali ya kampuni ya Buffalo kugongana na gari ndogo na kupinduka.
Akizungumzia ajali hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Handeni mkoani Tanga, Godwin Gondwe amesema kuwa tukio hilo limetokea leo Jumatano Agosti 14, 2019 katika kijiji cha Kwekwale na hakuna kifo chochote kilichotokea.
Amesema kuwa chanzo cha ajali hiyo ni dereva wa basi la Buffallo, Innocent Mauki kutaka kuyapita magari mengine mawili yaliyokuwa mbele yake huku eneo husika likiwa na alama za kukataza gari kumpita mwenzake.
“Naliagiza jeshi la polisi kumtafuta dereva wa hili basi halafu ashitakiwe kwa kosa la ku over take sehemu ambayo alama haziruhusu kufanya hivyo,”amesema DC Gondwe.
Lucas Karoli ambaye ni dereva wa gari ndogo yenye namba T 706 DPE amesema kuwa aliona dereva wa basi hilo akijaribu kuyapita magari mawili yaliyokuwa mbele yake huku alama zikiwa haziruhusu na ndio akaligonga gari lake upande wa kulia.
Kwa upande wao, abiria waliokuwepo kwenye ajali hiyo wametafutiwa gari nyingine na kuendelea na safari yao.
-
Waziri Mkuu azindua Mwongozo wa Uwekezaji mkoani Kagera
-
Mhadhiri NIT aburuzwa mahakamani kwa rushwa ya ngono
-
Ujumbe mzito watua mkoani Morogoro
CHANZO Mwananchi.