Wananchi wa Somalia wako katika wakati wa majonzi, wakichangisha fedha mitandaoni kwa ajili ya kuisaidia familia ya mwanaume aliyeuawa kikatili kwa kuchomwa moto kutokana na kuratibu mpango wa mpwa wake kumuoa binti wa kabila tofauti na lenye nguvu.
Ahmed Mukhtar Salah, alikuwa mjomba wa kijana wa kabila la Bantu, kijana ambaye alimchumbia kwa siri binti wa familia ya kabila tofauti na lake na lenye nguvu nchini humo.
Imeeelezwa kuwa baada ya wachumba hao kuondoka kwenda pasipojulikana kukwepa mkono wa ndugu wa mwanamke ambao walionesha kukasirishwa na uhusiano huo, familia ya mwanamke huyo ilimfuata Ahmed na kumtaka afanye kila liwezekanalo kumrejesha binti yao.
Lakini wiki iliyopita, Ahmed alikutwa akiwa amechomwa visu na kuchomwa moto hadi kufa katika jiji la Mogadishu.
Polisi wanamshikilia mama wa binti huyo pamoja na watu kadhaa wakihusishwa na shambulizi hilo dhidi ya Ahmed.
Vyombo vya habari nchini humo vimeeleza kuwa idadi kubwa ya waombolezaji walifika katika mazishi ya Ahmed Jumapili iliyopita, na baadaye kuanzisha mpango wa kuichangia familia yake kupitia mtandao maarufu wa kuchangisha fedha ‘GoFundMe’.
Ahmed alikuwa na familia ya watu 12 na alikuwa akifanya kazi ya ufundi wa magari.
Taasisi ya Somali Faces ambayo imeratibu mpango wa kumchangia Ahmed, ambapo hadi sasa umekusanya $3,211, lengo likiwa kukusanya $13,000.
Taasisi hiyo pia imeanzisha programu ya kutoa elimu kwa umma kuhusu ubaguzi wa makabila ambayo inaitwa ‘Sisi sote ni Sawa’ (We are all equal).