Paschal Misana, mkaazi wa kata ya Kinaga, Kahama Mkoani Shinyanga amechunwa ngozi ya uume na watu ambao hawajajulikana, kisha kutoweka nayo.
Akizungumzia tukio hilo, Misana ambaye amelazwa katika hospitali ya Mji wa Kahama, alisema kuwa anachokumbuka, aliitwa na mtu mmoja ambaye alikuwa anamdai shilingi 200,000 na alifika nyumbani kwake akiamini amemuita ili amlipe.
Anasema baada ya kufika aliwakuta watu watatu chumbani, wawili kati yao ni wanawake. Alipokelewa baiskeli yake iliyowekwa chumbani, baada ya kula ugali alipewa pombe aina ya shujaa na ndicho pekee alichokumbuka akiwa na watu hao.
Misana anasema kuwa baada ya kuzinduka alisikia maumivu makali sehemu zake za siri akiwa anasaidiwa na wasamaria wema pamoja na mke wa mdeni/mwenyeji wake huyo.
“Sikujua chochote, baada ya watu kujaa, wasamaria wema na kuanza kunipa huduma ya kwanza, walinielezwa kuwa shemu zangu za siri zlikuwa zimekatwa, hali iliyonishtua na baadaye polisi walifika wakanichukua na kunipeleka hospitalini,” alisimulia akiwa hospitalini hapo.
Mganga wa zamu wa Hospitali ya Mji wa Kahama, Dkt Abdallah Simba amesema kuwa Misana alifikishwa hospitalini hapo juzi mchana akiwa na hali mbaya, akivuja damu nyingi sehemu za siri kutokana na kitendo hicho.
“Wachunaji hao walimkata kitaalam kwani hawakufikisha kwenye mishipa ya sehemu za siri na hivyo tayari ameshonwa na kurudishiwa alipokuwa amekatwa wakati wa kuchunwa,” Mwananchi linamkariri Dkt Simba.
Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Simon Haule amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba wanamshikilia mtuhumiwa ambaye alikuwa mdeni wake, kwa ajili ya mahojiano.
Kamanda Haule amesema mtuhumiwa huyo ameliambia jeshi hilo kuwa wageni wake ndiyo walimchuna Misana na kisha walitoweka na hajui walikoelekea.