Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa ameahidi kufika katika ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kufuatia sakata la Fatuma Chikawe mwenye umri wa miaka 31 aliyedai kuwa ni mwanaye aliyemtelekeza.

Akizungumza hivi karibuni na gazeti la Nipashe, Makonda amesema kuwa Lowassa alizungumza na mmoja kati ya wanasheria wake kwa njia ya simu na kuahidi kufika katika ofisi hizo.

“Jana (juzi) Lowassa alizungumza na mwanasheria wetu kwa njia ya simu na amekubali kuwa atakuja ofisini kwangu,” Makonda anakaririwa na kuongeza kuwa Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo yuko nchini Ujerumani kwa matibabu hivyo watakutana akirejea.

Mkuu huyo wa Mkoa alisema kuwa aliagiza kukamatwa kwa mwanamke huyo kwakuwa aliikashfu ofisi yake kwa maneno aliyoyasema kwenye kipande cha video akijutia alichokifanya kuhusu Lowassa.

Makonda alisema kuwa Fatuma aliachiwa kwa dhamana baada ya kufuata taratibu za kisheria lakini baadaye familia ya Lowassa ilifika na kuzungumza naye ambapo walikubaliana watalimaliza suala hilo nje ya taratibu za kisheria.

Hata hivyo, Makonda alisema kuwa katika video aliyorekodi Fatuma, hakukubali au kukataa madai kuhusu Lowassa kuwa baba yake aliyemtelekeza lakini aliomba radhi kwa kilichokuwa kinaendelea baada ya kuwasilisha madai yake.

Awali, Lowassa alifanya mahojiano kwa njia ya simu na waandishi wa habari na kukana kumfahamu Fatuma. Alidai kuwa madai yake hayana ukweli na yanatumika kumchafua kisiasa.

Achunwa ngozi ya uume na ‘wasiojulikana’
Magazeti ya ndani na nje ya Tanzania leo Aprili 19, 2018