Aliyekua Mwenyekiti wa Klabu ya Simba SC, Ismail Aden Rage ameupongeza Uongozi wa sasa wa klabu hiyo kwa dhamira yao ya kutaka kuuendeleza Uwanja wa Mo Simba Arena uliopo eneo la Bunju jijini Dar es salaam.
Afisa Mtendaji Mkuu Barbara Gonzalez amewahi kuririwa na vyombo vya habari akisema wapo katika katika mpango mkakati wa kuendeleza ujenzi wa Uwanja wa Mo Simba Arena, na pesa zitakazopatikana kwenye Kampeni ya ‘Nani Zaidi’ zitatumikwa kwenye ujenzi huo.
Rage amesema, hana budi kuupongeza Uongozi wa Simba SC kwa juhudi walizozionesha hadi kufikia hatua ya timu ya klabu hiyo kuwa na eneo la kufanyia mazoezi.
Amesema ni hatua kubwa kwa klabu kama ya Simba SC kuwa na Uwanja wake wa Mazoezi, tofauti na wakati akiwa madarakani, ambapo walitumia viwanja vya kukodi kwa gharama kubwa kwa kila siku.
“Niwapongeze viongozi wa Simba SC kwa juhudi za kuhakikisha timu yetu imekua na eneo la kufanyia mazoezi, wakati mimi nipo madarakani eneo la Bunju lilikuwa pori na halikua na kitu chochote, lakini kwa msaada wa wanachama na Uongozi leo kuna jambo limefanyika.”
“Niwaombe viongozi wangu, wahakikishea wanatumia mapesa wanayoyapata kwa mwaka mzima kuendeleza kile kiwanja kwa sababu kwa sasa tunatumia gharama kubwa kwa kuiweka kambini timu yetu, ninaamini kama haya wanayoyafanya sasa watayafanikisha Simba SC itakua mbali na itapiga hatua kubwa” amesema Rage.
Leo Jumanne (Juni 14) Afisa Mtendaji Mkuu wa Simba SC Barbara Gonzalez alitembelea eneo la Uwanja wa Mo Simba Arena lililopo Bunju jijini Dar es salaam, akiongozana na msanifu majengo (architect).
Barbara alisema, zoezi la kujenga majukwaa na miundo mbinu mingine ya Uwanja wa Mo Simba Arena wamelidhamria na zimebaki siku chache kabla ya Bodi ya Wakurugenzi itakayokutana Ijumaa (Juni 17) ili kumpitisha mkandarasi.