Saa 24 baada ya Msemaji wa klabu ya Young Africans Haji Sunday Ramadhan Manara kuweka wazi namna anavyochukizwa na dhihaka anazozipata kutoka kwa baadhi ya watu nchini Tanzania kwa kigezo cha ulemavu wake wa ngozi, Mchambuzi wa Michezo kupitia Kituo cha EFM Radio Jemedari Said Kazumari amempa somo kwa kumtaka aache kuwadhihaki wengine.

Jemedari ambaye kwa sasa hana maelewano na Haji Manara ametumia Kurasa zake za Mitandao ya Kijamii kumfikishia ujumbe huo hasimu wake, huku akianza na maneno mazuri ya kuunga mkono kauli ya Manara kupinga dhihaka dhidi ya watu walemavu.

Jemedari ameandika: WATANZANIA TUBADILIKE, HII SIO SAWA..!

Ukimsikiliza Afisa Mhamasishaji wa Yanga utaona namna gani anaumizwa na dhihaka anayofanyiwa na Watanzania wenzake ambayo hajawahi kufanyiwa akiwa nje ya Nchi yake pendwa aliyozaliwa na kuipenda.

Kama kuna Watanzania wanamfanyia dhihaka hii bila sababu yoyote, yani anapita tu mtaani unamdhihaki kwa ulemavu wake wanakosea sana sana sana.

Hatupaswi kufanya namna hiyo kwani jamii na familia zetu zinatufundisha kuwa na huruma na watu wenye mapungufu ya kimaumbile kwa namna yoyote ile.

Watanzania wanapaswa kufuata mafundisho mema ya Dini zetu Kuu 2 ambazo zote zinapinga hili kama zinavyopinga mambo mengi maovu yasiyo na maana.

Mytake

Ulemavu haupaswi kuwa kinga kwa mmoja wetu kufanya dhihaka kwa wengine kisa yeye mlemavu, akidhihakiwa yeye kwa ulemavu wake ama namna nyingine yoyote, aanze kusaka huruma ya jamii.

Afisa mhamasishaji amedhihaki wangapi kwa maumbile yao? Alimdhihaki Makamu Mwenyekiti wa Yanga na kumuita Kilo 800 tena mbele ya Camera za Waandishi Habari, huko alikotembea mwenzetu ile ni sawasawa tu.

Afisa mhamasishaji amemdhihaki mara ngapi mwekezaji wa Simba kwa Uhindi wake? Vipi huko Duniani wanakoenda wenzetu hii haina shida? Wangapi wamedhihakiwa na kuitwa majina yasiyofaa iwe dhahiri au kwa kificho na Bwana huyu ambaye analalamika yeye kudhikiwa?

Ukidhihaki wenzio kwa unayoyaona yanafaa kwako, usiwachagulie wewe wakudhihaki kwa lipi. Dawa ni kutowadhihaki ili nawe wakulindie udhaifu wako.

Vingenevyo kuwa mvumilivu tu bro, kuna walemavu wa ngozi wanapaswa kulalamikia hilo lakini sio wewe au wale wenye tabia kama zako, kwani unaowadhihaki ni Binadamu kama wewe wana wazazi, mioyo, ndugu na familia kama wewe. Wanaumizwa na dhihaka zako ila wanavumilia wao na familia zao, nawe vumilia tu usitangulize ulemavu wako

Mwalimu wa Madrasa anaejua Dini vilivyo hawezi kuwa wa mwanzo kutakia wengine mabaya tena hadharani na kushinda kwenye vilabu vya pombe analewa halafu analalamika jamii yake kukosa Dini. Nani anapaswa kuwa mfano sasa kama sio wanazuoni wa mambo ya Dini?

NB: Ukiishi kwenye nyumba ya vioo usiwe wa kwanza kuanzisha ugomvi wa mawe, wajuba watakupopoa tu bila kujali mambo mengine.
BIN KAZUMARI.

Aden Rage aupongeza Uongozi Simba SC
Idadi ya vifo yafikia 79, Rais atangaza maombolezo