Meneja wa klabu ya Manchester United Jose Mourinho huenda akakwepa hatua za kinidhamu, baada ya kuondolewa kwenye benchi la ufundi wakati wa mchezo wa ligi dhidi ya Southampton siku ya jumamosi.
Mourinho mwenye umri wa miaka 54, aliondolewa katika benchi la Man Utd na mwamuzi Craig Pawson, baada ya kuvuka eneo lake la kutoa maelezo kwa wachezaji wa Man Utd na kuingia sehemu ya uwanja.
Hata hivyo adhabu ya meneja huyo kutoka nchini Ureno imekua kizungumkuti na kuibua hisia tofauti kwa wadadisi wa soka kutokana na tukio lilivyokua.
Wapo wanaodai kuwa, Mourinho hatofanywa lolote na FA, kutokana na kuafiki adhabu aliyopewa wakati wa mchezo, na wengine wanadai huenda akachukuliwa hatua za kinidhamu.
Lakini kama mwamuzi Pawson atakua ameliainisha tuko hilo kwenye ripoti yake aliyoituma FA baada ya mchezo, kutakua na sababu kwa Mourinho kuadhibiwa, kwa kutokukaa katika benchi la ufundi katika michezo kadhaa ya ligi.
Wakati huo huo chama cha soka nchini England (FA), kinatarajiwa kutoa kalipio ama adhabu kwa mashabiki wa Southampton, kufuatia matukio ya kibaguzi dhidi ya mshambuliaji wa Man Utd Romelu Lukaku.
Tayari uongozi wa klabu ya Southampton umeshaanza kufanya uchunguzi wa kina kupitia kamera za CCTV, ili kuwabaini mashabiki waliokua wakiongoza vitendo hivyo vya kibaguzi.