Mahakama ya juu nchini Saudi Arabia imetangaza kufuta adhabu ya viboko na kusema hatua hiyo ni moja ya mageuzi muhimu katika kulinda haki za binadamu yaliyofanywa na mfalme Salman na mtoto wake wa kiume Mohamed.
Mahakama hiyo imesema mageuzi yaliyofanyika yanalenga kuifanya Saudi Arabia kuwa falme inayoheshimu desturi za kimataifa kuhusu halki za binadamu zinazopinga adhabu za viboko.
Kwa miaka mingi amri za mahakama za kuwacharaza wahalifu viboko ambavyo vilikuwa vinaweza kufikia idadi ya 100 zimekuwa zikipingwa vikali na makundi ya kutetea haki za binadamu.
Mahakama nchini Saudi Arabia zimekuwa zikitoa adhabu ya viboko kwa watu waliotiwa hatiani kwa makosa ikiwemo kufanya mapenzi nje ya ndoa, kuvuruga amani na hata mauaji.