Mabingwa mara nne wa Afrika, timu ya taifa ya Cameroon wametinga kwenye hatua ya fainali ya michuano ya AFCON 2017, kwa kuwabamiza Ghana mabao mawili kwa sifuri.
Cameroon ambao walikuwa wakipewa nafasi finyu ya kutinga kwenye hatua hiyo, walionyesha soka safi katika mchezo wa nusu fainali ya pili uliochezwa usiku wa kuamkia hii leo mjini Franceville nchini Gabon.
Mabao ya ushindi ya Cameroon yalipachikwa wavuni mwa Ghana na Michael Ngadeu-Ngadjui na Christian Bassogog katika dakika ya 72 na 90.
Ushindi wa Cameroon umeendeleza maumivu ya Ghana ya kukosa ubingwa wa Afrika kwa miaka 35.
Kwa mara mwisho Ghana walitwaa ubingwa wa fainali za Afrika mwaka 1982.
Cameroon wameingia hatua ya fainali wakiwa na lengo la kutaka kutwaa ubingwa wa Afrika kwa mara ya tano huku wapinzani wao Misr,i wakihitaji kuendeleza rekodi ya kuendelea kuwa wafalme wa kihistoria kwa kusaka taji la nane.
Mara ya mwisho timu hizo mbili zilikutana katika hatua ya fainali mwaka 2008, na Cameroon walikubali kufungwa bao moja kwa sifuri.