Majogoo wa Jiji Liverpool wameanza kuwaza namna gani mambo yatakavyokuwa upande wao kwenye Ligi Kuu England msimu ujao baada ya kuwa kwenye hatari ya kukosa huduma ya supastaa wao matata, Mohamed Salah, ambaye atakuwa kwenye majukumu ya kulitumikia taifa lake kwenye michuano ya AFCON 2024.
Liverpool ilimaliza msimu wa 2022-23 hovyo kwelikweli, hivyo haitahitaji kurudia jambo hilo, lakini hofu inaibuka kwa kuwa itakwenda kumpoteza Mo Salah katika kipindi muhimu cha msimu.
Baada ya ratiba mpya ya Ligi Kuu England kutoka, Liverpool itakwenda kumkosa Mo Salah kwenye mechi nne mwanzoni mwa mwaka 2024, ambapo michuano hiyo ya ubingwa wa Afrika itafanyika.
Idadi ya mechi hizo zinaweza kuongezeka kama Misri itavuka hatua ya makundi, kitu ambacho ni kawaida kwa upande wao kutokea.
Kwa kipindi hicho cha kuanzia Januari hadi Februari, kumekuwa kukifanyika pia mechi za Raundi ya Tatu ya Kombe la FA, ambapo mechi hiyo ratiba yake inaweza kupangwa siku sita kabla ya kuanza kwa Afcon 2024.
Kwenye Ligi Kuu England, mechi ambazo Mo Salah anaweza kuzikosa ni pamoja na Chelsea na Arsenal ambazo zitafanyika Februari, endapo kama chama la Misri litafika hatua za juu kabisa kwenye michuano ya Afcon 2024.
Kocha Jurgen Klopp atatumainia huduma za wachezaji kama Luis Diaz na Diogo Jota kuchukua mikoba ya Mo Salah kwa kipindi ambacho atakosekana kwenye kikosi hicho.