Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Stergomena Tax ameshiriki maadhimisho ya miaka 60 ya Umoja wa Afrika. Maadhimisho hayo ya miaka 60 ya Umoja wa Afrika yalifanyika jijini Dar es Salaam tarehe 25 Mei, 2023 na kuhudhuriwa na Jumuiya ya Mabalozi wa nchi za Afrika na Taasisi za Kimataifa za Afrika zilizoko nchini.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Dkt. Tax alitoa rai kwa nchi za Afrika kuungana ili kukua na kuwa na uchumi imara na kuongozwa na misingi na mawazo ya kuunganisha waafrika na hivyo kudumisha amani na usalama na kupata maendeleo ambayo yatatokana na utambulisho wake, urithi wa pamoja, maadili ya pamoja, mitazamo na ubunifu wa watu wake.
Amesema, “Afrika lazima ijengwe kwa kuungana ili ishamiri, iwe na uchumi imara na kuongozwa na misingi ya kuunganisha waafrika ili kulinda amani na usalama ambayo maendeleo yake yanatokana na utambulisho wake yenyewe, urithi wa pamoja, maadili ya pamoja, mitazamo na ubunifu wa watu wake.”
Aidha, Dkt. Tax pia amezisihi nchi za Afrka kutumia vizuri fursa za kiuchumi zilizopo ili kwa kuchochea ufanyaji biashara miongoni mwao na kufikia azma ya utekelezaji wa malengo ya Agenda 2063 na kwamba Afrika ni bara la pili kwa ukubwa likiwa na watu zaidi ya bilioni 1.2 na hivyo kuwa na fursa mbalimbali ambazo zikitumiwa vizuri zitawezesha waafrika kufikia azma ya utekelezaji wa Agenda 2063.