Mahakama ya Afrika Kusini imeamuru kushikiliwa kwa nyumba ya Nabii na Mchungaji milionea wa raia wa Malawi Shepherd Bushiri anayehubiri nchini Afrika Kusini, baada ya Nabii huyo na mkewe Mary kukwepa kesi ya dhamana.
Kwa mujibu wa taarifa, kasri hiyo ya kifahari iliyopo karibu na mji wa Pretoria ina thamani ya randi milioni 5.5 za Afrika Kusini sawa na dola 350,000 yaani zaidi ya shilingi Millioni 800 za kitanzania.
Jaji aliwaamuru Nabii Bushiri na mke wake kutoa stakabadhi za nyumba wakati mahakama hiyo ilipowapa dhamana kufuatia tuhuma za utakatishaji wa fedha na ufisadi zinazowakabili.
Hatua hii ya mahakama inakuja wakati Mchungaji huyo maarufu akikabiliwa na mashitaka 419 na utakatishaji wa fedha nchini Afrika Kusini.
Wakati huo huo mahakama ya Malawi imemuachilia huru Nabii Shepherd Bushiri na mke wake na Afrika Kusini bado inawataka Bushiri na mke wake ambao walitorokea nchini kwao Malawi warejee Pretoria kukabiliana na mashitaka dhidi yao.
Bushiri na mke wake ambaye pia ni Nabii wamekanusha tuhuma dhidi yao, kupitia ujumbe walioutuma kwenye mitandao ya kijamii wakidai walikuwa nchini Malawi kwa kuhofia usalama wao.