Msemaji Mkuu wa Serikali ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbas amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano chini Rais John Magufuli itatengeneza wasanii maarufu na matajiri, miaka mitano mingine.

Akizungumza katika mahojiano maalum na Dar24 hivi karibuni bungeni jijini Dodoma, Dkt. Abbas alisema kuwa hotuba ya Rais Magufuli imeweka nia madhubuti ya kuwanufaisha wasanii, kilichobaki ni watendaji kuhakikisha inatimia.

 “Mheshimiwa Rais ametupatia changamoto kwamba anataka kuona wasanii wananufaika na kazi zao. Unajua sasa hivi wasanii wengi ni maarufu lakini maskini. Kwahiyo tuendako, nimeweka msemo ‘tunataka wasanii maarufu lakini matajiri. Na huko ndiko tunakokwenda,” amesema Dkt. Abbasi.

Ameongeza kuwa Rais Magufuli ameshaweka nia ya kisiasa na kazi imebaki kwa watendaji kuhakikisha wanatekekeleza nia hiyo.

Akizungumzia njia atakayotumia kufikia malengo, Dkt. Abbas amesema ataanza ziara ya kukutana na wadau wa sanaa na ili kutengeneza mambo ambayo wangependa yafanyiwe kazi.

“Hili nalisema kwa mara ya kwanza hapa Dar24… kuanzia wiki ijayo naanza hiyo ziara, tutengeneze mambo makubwa labda tuseme matano au kumi, tumpelekee mheshimiwa Rais, kwamba ‘mheshimiwa kwenye sekta ya sanaa ukitufanyia haya kumi umetutoa, hicho ndicho nachotaka na kitoke kwa wasanii wenyewe,” Dkt. Abbas ameiambia Dar24.

Amesema anataka kuwasikiliza wadau wa sanaa wanataka nini kiuhalisia, na kwamba atazungumza na wadau wote kuanzia wasanii, DJs, watayarishaji wa muziki, wachoraji n.k, na changamoto zao pamoja na mapendekezo yao yatatengeneza njia halisi ya kupata ufumbuzi.

Aidha, Dkt. Abbas amesema kuwa tayari ufumbuzi wa kwanza umeshafanyika, ambapo Mfuko wa Maendeleo ya Sanaa ameshauanzisha, kuwawezesha wasanii kupata mitaji na mikopo.

“Lakini pia wasanii wanataka kuendelezwa kwenye kazi zao… sasa mimi nikwambie tu rasmi kwamba hapa tunavyozungumza huo mfuko nimeshauanzisha… taarifa kamili nitaitoa baadaye lakini uchukue tu kwanza kwenye Dar24… Mfuko wa Maendeleo ya Sanaa tayari nimeshauanzisha,” amesisitiza.

Mfuko huo ulikuwa sehemu ya hotuba ya Rais Magufuli, ambaye alisema Serikali itaanzisha mfuko huo kwa ajili ya kuwasaidia wasanii.

Tanzania: Watu nane huambukizwa VVU kila baada ya saa moja
Maalim Seif ajibu baada ya kupokea barua ya Rais Mwinyi

Comments

comments