Mahakama ya Hakimu mkazi Mkoa wa Tabora imemuhukumu kutumikia kifungo cha miaka 30 jela kijana aliyefahamika kwa jina la Rwaki Zakaria baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka mwanafunzi wa darasa la sita anayesoma Shule ya Msingi Kigwanhona katika Kijiji cha Kigwanhona Wilayani Uyui na kumsababishia ujauzito.
Wakili wa Jamhuri, John Nkonyi amesema mshtakiwa alitenda kosa hilo kati ya Januari na Februari mwaka huu kinyume na Kifungu cha 60 cha Sheria ya Elimu Sura ya 353 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2019.
Mshtakiwa huyo alikuwa akimchukua mwanafunzi huyo anayeishi na Bibi yake na kwenda nae porini na kumbaka mara kwa mara na kisha kumrudisha nyumbani hadi kufikia hatua ya kumpa ujauzito na kusababisha kukatishwa masomo binti huyo.
Hakimu mkazi katika Mahakama hiyo ya Tabora, Ajali Milanzi baada ya kupitia ushahidi wa watu wanne wa upande wa mlalamikaji na ushahidi uliotolewa na mshtakiwa, amesema mahakama ilijiridhisha pasipo shaka yoyote kwamba mshtakiwa amehusika kutenda kosa hilo la jinai na kumhukumu kutumikia kifungo cha kwenda jela miaka 30.
Mahakama pia imetoa nafasi kwa mshtakiwa kutafuta haki yake kwa kukata rufaa, endapo hataridhika na hukumu hiyo.