Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amefika kata Murusagamba Wilayani Ngara Mkoani Kagera kufatia agizo alilopewa na Naibu waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Dotto Biteko Septemba 29, 2023 la kuleta suluhisho la upatikanaji wa maji katika maeneo hayo.
Aweso amesema tayari Wizara ya Maji imetoa shilingi milioni 250 kwaajili ya kuanza kutekeleza mradi wa maji katika kijiji cha Murusagamba na kumtaka mkuu wa wilaya ya Ngara Kanali Mathias Kahabi kutumia wafungwa kuchimba mitaro ili ndani ya siku 30 mradi huo uwe umekamilika na kukabidhiwa kwa wananchi.
Amesema, kutokana na ongezeko la wa tu katika kijiji cha Murusagamba kumepelekea huduma ya maji kuwa hafifu hivyo mradi huo utawekewa miundombinu mipya ili maji yawafikie wananchi kwa urahisi huku akimuagiza Meneja wa RUWASA Mkoa wa Kagera, kutangaza mradi wa maji wa kijiji cha Ntanga wenye gharama zaidi ya shilingi milioni 700.
Aidha, ameagiza Mkandarasi anayetekeleza mradi wa maji wa Kumubuga kufika ofisi za mkuu wa wilaya kutoa maelezo ya lini anamaliza mradi anaoujenga kutokana na kuchelewa kwa mradi huo.