Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba SC Ahmed Ally ameshindwa kuficha hisia zake, baada ya Watani zao wa Jadi Young Africans kupoteza mchezo wa kwanza msimu huu dhidi ya Ihefu FC.
Young Africans ilipoteza mchezo huo jana Jumanne (Novemba 29), ikicheza ugenini Uwanja wa Highland Estate Wilayani Mbarani Mkoani Mbeya, kwa kufungwa mabao 2-1 na kuangusha alama tatu kwa mara ya kwanza baada ya kucheza michezo 49 mfululizo bila kufungwa.
Ahmed Ally amesema hawana budi kuipongeza Ihefu FC kwa matokeo hayo ambayo waliyasubiri kwa muda mrefu, kwa sababu wameifanya Ligi Kuu kuendelea kuwa na ushindani wa karibu.
“Tunawapongeza sana Ihefu kwa ushindi. Sisi kama Simba tumefurahi sana. Ihefu wanapaswa kupongezwa sana wamefanya jambo kubwa sana na ushindi walistahili”
“Matokeo haya tuliyasubiri kwa muda mrefu sana. Tumefurahi zaidi kwa sababu gape letu na wale jamaa limepungua, tunawashukuru sana Uhefu kwa kuwapunguza speed”
“Tunaamini kabla ya mzunguko wa kwanza kuisha tutakuwa tumewafikia” amesema Ahmed Ally
Hata hivyo Young Africans inaendelea kuongoza msimamo wa Ligi Kuu kwa kuwa na alama 32 baada ya kucheza michezo 13, ikifuatiwa na Azam FC yenye alama 32 huku Simba SC ikishika nafasi ya tatu kwa kuwa na alama 31.
Ihefu FC imesogea kwa nafasi tatu kutoka nafasi ya 16 hadi ya 13, ikifikisha alama 11, baada ya kucheza michezo 14.