Klabu ya Simba SC imesema Soka ambalo lilipigwa kwenye mchezo wa Mkondo wa Pili wa Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Wydad AC ya Morocco, ndio watakaouonyesha kwenye mchezo wa Nusu Fainali Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ dhidi ya Azam FC.
Kauli hiyo ya tambo kwa Simba SC imetolewa na Meneja Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ally, huku akilishukuru Shirikisho la Soka nchini (TFF), kwa kuusogeza mbele mchezo huo kutoka Jumamosi (Mei 06) mpaka Jumapili (Mei 07).
Mchezo huo umepangwa kupigwa katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara kuanzia saa kumi jioni, huku timu zote zikitarajiwa kuwasili mjini humo kuanzia leo Ijumaa (Mei 05).
Ahmed, ameitahadharisha Azam FC kukutana na Simba SC ambayo kwa sasa ipo kwenye kiwango cha juu sana cha soka si la Tanzania, bali Barani Afrika.
“Ni mchezo muhimu sana kwetu, ni ya kutupeleka fainali na kama tutacheza kama tulivyocheza dhidi ya Wydad Casablanca mpaka mashabiki wa timu hiyo wakaufanya uwanja kuwa sehemu ya kufanyia sala, Azam FC anatusumbuaje? Na itakuwa ni maajabu makubwa, unampelekea pumzi ya moto Wydad ya Morocco, halafu anakuja mtu kutoka Chamazi kukusumbua kweli, yatakuwa ni mambo ya kushangaza dunia,” amesema Ahmed.
Amesema kwenye mchezo huo wanataka waihakikishie dunia kuwa kile ndicho kiwango chao halisi na wala hawakubahatisha, na kama watacheza kwa asimilia 80 tu, basi dhahama kubwa itawakumba Azam FC.
“Nikisema hivyo nina maana ni lazima tulinde kiwango chetu, hivi sasa tupo kwenye kilele cha ubora kwa hiyo kila mechi ni lazima tucheze kwa kiwango kile kile, si leo umecheza asilimia 80, kesho 20, keshokutwa 60, yaani inakuwa ni kama unabahatisha maisha hivi. “Tunatakiwa tucheze huku kila Mwanasimba akiwa ‘anainjoi’ Tunataka kuona mashabiki wetu wakiangalia mechi za timu yetu wawe kama wanaangalia tamthilia tamu ya mahaba, siyo unatazama mpira umeshikilia roho,” amesema
Awali, Simba na Azam zilikuwa zicheze mchezo huo, lakini TFF iliusogeza mbele, huku pia ikiuahirisha mwingine wa nusu fainali kati ya Young Africans na Singida Big Stars uliokuwa uchezwe Mei 7, kwenye Uwanja wa Liti, Singida, hadi utakapopangiwa tarehe nyingine, baada ya kulikubali ombi la Young Africans ambayo iliiomba mchezo huo usogezwe mbele ili kupata nafasi ya kujiandaa na mchezo wa Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya Marumo Gallants utakaochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, Mei 10, mwaka huu.