Uongozi wa Simba SC umeweka wazi kuwa nyakati ngumu ambazo wanazipitia kwa sasa zinawakomaza, hivyo wanaamini watarejea kwenye ubora wao kwa mechi zinazofuata.

Ipo wazi kuwa ndani ya Novemba Simba hajaambulia ushindi kwenye mechi tatu mfululizo za ushindani iliocheza, mbili za ligi ambazo ni dakika 180 na moja ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya ASEC Mimosas.

Katika mchezo uliopigwa juzi Jumamosi (Novemba 25) walikuwa nà matumaini ya kukomba pointi tatu kutokana na bao la kipindi cha kwanza lililofungwa na Saido Ntibanzokiza dakika ya 44, ila mwisho ngoma iliisha ikiwa sare yaani Simba 1-1 ASEC Mimosas.

Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally amesema kuwa kazi kubwa bado ipo kutokana na kushindwa kupata matokeo kwenye mchezo wa kwanza wakiwa nyumbani.

“Malengo ilikuwa ni kupata pointi tatu kwenye mchezo wetu, kwa kuwa imeshindikana basi tutapambana kwa mechi zinazofuata. Nyakati ngumu ambazo tunapitia zinatukomaza hivyo tutakuwa imara.

Mashabiki wazidi kuwa pamoja nasi kwenye mechi ambazo tunacheza kama ambavyo sera yetu inasema, nguvu moja tutambana kwenda kwenye mwendo wetu, amesema Ally.

Mchezo ujao wa Simba SC ni dhidi ya Jwaneng Galaxy unatarajiwa kuchezwa Desemba 2, ambapo Mnyama atakuwa ugenini.

Kisa Nigeria: Niger yaanza kutumia Umeme wa jua
Agizo la Waziri Mkuu lawasilishwa kwa Wakurugenzi