Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Ahmed Ally amewajibu baadhi ya wadau wa soka nchini wanaopinga hatua ya wachezaji wa kimataifa kufanyiwa majaribio kupitia Michuano ya Mapinduzi.
Simba SC imetumia michuano hiyo kuwafanyia majaribio wachezaji wa kimataifa Etop David Udoh (Nigeria), Sharaf Eldin Shaiboub Ali Abdelrahman (Sudan) na Moukoro Cheik Tenana (Ivory Coast), ambao huenda wakasajiliwa kupitia Dirisha Dogo la Usajili ambalo rasmi litafungwa Jumamosi (Januari 15).
Akizungumza na Dar24 Media #taarifabilamipaka mjini Unguja-Zanzibar Ahmed amesema, hatua ya kufanya majaribio kwa wachezaji hao sio dhambi, na dhumuni la benchi la ufundi la Simba SC ni kuhakikisha linapata mchezaji ambaye atakidhi vigezo.
Amesema Simba imewahi kufanya majaribio ya wachezaji kadhaa huku akimtaja aliyewahi kuwa Nahodha na Beki tegemeo wa Young Africans Lamine Moro, na matokeo yake beki huyo alishindwa kufikia vigezo walivyohitaji.
“Niwakumbushe Simba SC tumewahi kuwafanyia majaribio wachezaji wengi sana hapa nchini, tumefanya kwa Lamine Moro ambaye kwetu hakuonekana anafaa, lakini kwa wenzetu walitumia mpango wetu na walimsajili na kisha walimpa hadi unahodha,”
“Kipindi hiki cha Dirisha Dogo tumeona tuitumie michuano ya Mapinduzi kuwafanyia majaribio hawa wachezaji na tumefanikiwa, huu ni mfumo wetu sisi kama Simba SC kama wengine hawautumii basi, lakini sisi tunajua tunachokifanya kupitia kwa kocha wetu Franco Pablo Martin.” Amesema Ahmed Ally.
Baada ya mchezo wa Fainali wa Kombe la Mapinduzi utakaochezwa kesho Alhamis (Januari 13) dhidi ya Azma FC, Kocha Mkuu wa Simba SC Franco Pablo Martin anatarajiwa kuwasilisha maamuzi yake kwa viongozi wa Simba SC baada ya kuwafanyia majaribio Etop David Udoh (Nigeria), Sharaf Eldin Shaiboub Ali Abdelrahman (Sudan) na Moukoro Cheik Tenana (Ivory Coast).