Meneja wa Habari na Mawasiliano Simba SC, amepingana na baadhi ya Mashabiki na Wanachama wa Klabu hiyo ambao hawakupendezwa na maamuzi ya Kocha Robertinho ya kumtoa Clatous Chama, na kumpa nafasi Kibu Denis wakati wa mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Mbeya City.
Simba SC iliyokua nyumbani juzi Jumatano (Januari 18), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, iliibuka na ushindi wa mabao 3-2 na kufikisha alama 47, kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ikitanguliwa na Young Africans yenye alama 53.
Ahmed Ally amesema baadhi ya Mashabiki na Wanachama walishindwa kueleza mpango kazi wa Kocha Robertinho wa kumtoa Chama Uwanjani, na kujikuta wakibua malalamiko ambayo anaamini majibu yake yalijibiwa pale pale Uwanjani.
Amesema Kocha huyo kutoka nchini Brazil alijiridhisha kuwa Chama hakulazimika kuendelea kuwepo Uwanjani, na ndio maana alifanya maamuzi ya kumtoa bila kujali kelele za Mashabiki na Wanachama, ambao wamezoea kumuona Mchezaji huyo kutoka Zambia akicheza mara kwa mara tena kwa dakika zote.
“Watu wote waliokuwa uwanjani na waliokuwa wanatazama kupitia TV tulishtuka kuona Kocha Robertinho anamtoa Chama!”
“Baada ya kushtuka kuna watu ambao tukaamua kusubiri kuona Kocha anataka kufanya nini halafu wapo waliosema huyu Kocha hatufai! Waliosema huyu Kocha hatufai hadi sasa hivi wameshikilia msimamo huo.”
“Tulioamua kusubiri kuona kocha atafanya nini alitujibu palepale uwanjani, baada ya muda mfupi tukaona kwa nini aliamua kufanya mabadiliko yale.”
“Maamuzi aliyoyafanya ni kwa maslahi ya timu, kwa jicho lake la kiufundi aliona pamoja na ubora wote wa Chama lakini kwenye mchezo ule alihitaji mtu mwingine.”
“Kiutawala sisi tumefurahi kuona tuna mwalimu ambaye anaweza kufanya maamuzi magumu! Kwenye maisha huwezi kufanikiwa kama huwezi kufanya maamuzi magumu.” amesema Ahmed Ally
Hata hivyo kabla ya kutolewa Uwanjani, Chama aliisaidia Simba SC kupata bao la kuongoza, kufuatia pasi ya mwisho aliyompigia Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Burundi Saido Ntibazonkiza aliyefunga mabao mawili kwenye mchezo huo.