Meneja wa Habari wa Simba SC, Ahmed Ally amesema kikosi chao kina nafasi kubwa ya kuonyesha mchezo safi leo jumatano (Januari 26) dhidi ya Kagera Sugar, kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.

Simba SC iliwasili Bukoba jana Jumanne (Januari 25) mchana ikitokea Dar es salaam kwa ajili ya mchezo huo wa kiporo ambao ulipaswa kuchezwa Desemba 12 mwaka 2021, lakini uliahirishwa na Bodi ya Ligi kutokana na wachezaji wengi wa Simba SC kukutwa na maambukizo ya ugonjwa wa mafua, kukohoa, kichwa na homa kali, hivyo kusababishwa mechi isifanyike kwenye Uwanja wa Kaitaba.

Ahemd amesema maandalizi ya mchezo huo yameshakamilika na kinachosubiriwa kwa sasa ni muda wa mchezo, ambao utakua saa kumi jioni.

Amesema Simba SC ilishindwa kuonesha soka safi katika mchezo uliopita dhidi ya Mtibwa Sugar kutokana na Uwanja wa Manungu Complex kutokua rafiki, hivyo Uwanja wa Kaitaba unatoa fursa kwa wachezaji wao kucheza soka safi, ambao kwa hakika ana matumaini watapata ushindi na alama tatu muhimu.

“Kikubwa tunachofurahia ni kwamba tupo Bukoba kucheza katika Uwanja wenye hadhi yetu, kiwanja ambacho kinawapa fursa wachezaji wetu kuonesha ubora wao.”

“Hakuna asiyefahamu uwezo wa wachezaji wetu walioipa ubingwa wa ligi kwa miaka minne mfululizo siyo kitu kidogo, hivyo tuna matumaini mkubwa sana kwao, baadae watatupa matokeo na alama tatu muhimu hapa ugenini.” amesema Ahmed Ally

Simba SC iliyochezwa michezo 12 ya Ligi Kuu msimu huu inashuka Dimbani ikiwa na alama 25 zinazowapa nafasi ya kuwa wapili kwenye msimamo wa Ligi hiyo, huku wenyeji wao Kagera Sugar ambao pia wamecheza michezo 12 wakiwa na alama 13 zinazowaweka kwenye nafasi ya 11.

Mazanzala: Tuna nafasi ya kushinda leo
Hospitali za mipakani kutoa huduma za kibingwa