Baada ya Mlinda Lango chaguo la kwanza Simba SC, Aishi Manula kufanyiwa upasuaji wa nyama za paja utakaomweka nje kwa miezi minne, haraka mabosi wa Msimbazi wameanza kusaka Mlinda Lango mpya na hadi sasa mezani kwao kuna majina matatu kutoka nchi tofauti.
Manula alifanyiwa upasuaji huo wiki iliyopita nchini Afrika Kusini, baada ya kuumia katika mchezo wa robo fainali Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) dhidi ya Ihefu Aprili 7, mwaka huu kwenye Uwanja wa Azam Complex.
Taarifa ya Manula kukaa nje kwa miezi minne imeufanya uongozi wa Simba kuongeza kasi ya kusaka Mlinda Lango mpya mpya atakayeingia moja kwa moja katika kikosi cha kwanza mbele ya Ally Salim na Ahmed Feruz waliochipukia kutoka timu za vijana kikosini hapo.
Ikumbukwe msimu ujao Simba haitakuwa na huduma ya Beno Kakolanya ambaye inafahamika tayari amesajiliwa na Singida Big Stars na kilichobaki ni kutangazwa tu.
Ili kuhakikisha hawafanyi makosa katika usajili wa Mlinda Lango mpya, mabosi wa Simba sambamba na benchi la ufundi chini ya kocha mkuu Mbrazili, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ wamewekewa majina matatu mezani na Kamati ya Usajili ili kuyapitia kisha kuchambua kwa vigezo nani anayewafaa.
Mlinda Lango wa kwanza katika orodha hiyo ni Muivory Coast, Issa Fofana anayeidakika Al Hilal Omdurman ya Sudan inayonolewa na Mkongoman, Florent Ibenge.
Simba imeanza mazungumzo na Fofana ikitumia hali ya vita iliyopo mjini Omdurman iliyosababisha Ligi ya Sudan kusimama na wachezaji kupewa mapumziko yasiyo na muda maalumu wa kikomo.
Tayari mazungumzo kati ya Simba na wawakilishi wa Fofana yameanza na kama kila kitu kitaenda vizuri basi atatu Msimbazi.
Mlinda Lango wa pili ni raia wa Brazil aliyependekezwa na Kocha Robertinho na kummwagia sifa ni bora na anaweza kuisaidia Simba.
“Nina Mlinda Lango ambaye kama uongozi utakuwa tayari atakuja hapa, ni bora na anajua kila kitu kuhusu eneo lake, anaweza akawa namba moja kwenye timu yoyote Afrika na tukimpata Simba basi tatizo la Mlinda Lango litakuwa limeisha,” alisema Robertinho.
Hata hivyo, ni kama uongozi wa Simba bado unasikilizia maamuzi ya kumleta Mlinda Lango huyo nchini kutokana na kutokuwa na imani naye kwani haujawahi kumwona akicheza mechi zaidi ya picha na video zilizotengenezwa, pia hana uzoefu na soka la Afrika.
Mlinda Lango mwingine wa tatu ni Mrundi, Fabien Mutombora wa Vipers ya Uganda alikotoka Robertinho kabla ya kujiunga na Simba na tayari mazungumzo yameanza na inaelezwa Mlinda Lango huyo yupo tayari kujiunga na Wanamsimbazi.
Moja ya viongozi wa Simba (jina tunalo), amesema leo Jumatatu watakaa kikao na benchi la ufundi na kupitisha jina la Mlinda Lango mmoja kati ya hao waliotajwa ili asajiliwe mapema.
“Jumatatu ndio tutakuwa na kikao na benchi la ufundi kujua tunamsajili nani, wameletwa makipa wengi lakini hao watatu ndio wako msitari wa mbele kusajiliwa.
“Huyo Mbrazil na huyo wa Uganda kama wakipitishwa basi hawatakuwa na mchakato mrefu kuwapata lakini kwa Fofana itahitajika pesa na makubaliano ya pande tatu kwa maana ya Simba, Al Hilal na mchezaji mwenyewe,” kilisema chanzo chetu.
Kwa upande wa Robertinho alisema anataka Mlinda Lango atakayekwenda Simba kutoa changamoto kwa waliopo na kuongeza ushindani.
“Lazima tusajili Mlinda Lango mpya, tunataka kwenye kila eneo kuwe na wachezaji wasiopungua wawili wanaoshindana kwa hali ya juu, hivyo taratibu zinaendelea na naamini tutalitimiza hili mapema,” alisema Robertinho.