Na Josefly:
Billy Milligan, alizaliwa Februari 14, 1955, Miami Beach, Florida nchini Marekani. Wazazi wake walimpa jina la William, lakini maisha yakamuongeza jina la Billy. Huyu alikuwa binadamu wa ajabu kuishi katika Karne hii ya 21. Alibainika kuwa ndani yake kulikuwa na utu 24, yaani 24 personalities. Ni kama alikuwa anaishi na watu 24 tofauti ndani yake, akiwa na mwili mmoja. Ndani ya Billy Milligan kulikuw ana utu wa mwanamke, tu wa mtoto mdogo, utu wa mtu mpole na mnyenyekevu, utu wa mtu katili sana na mbakaji, na ilibainika alikuwa na watu 24 ndani yake ambao walifanya matendo mengi bila idhini yake.
Unaweza kuangalia video zaidi hapa kufahamu watu watano wa ajabu zaidi kuwahi kutokea:
Hii ilibainika baada ya kukamatwa na kufikishwa mahakamani akiwa amefanya matukio ya mauaji na ubakaji kwa nyakati tofauti. Kwa bahati nzuri, aliowafanyia matukio ya ubakaji walitoa ushahidi uliothibitisha kuwa dakika chache kabla ya tukio walimuona akiwa katika utu tofauti kabisa. Na kwamba aliye mbele yao ni mtu tofauti na yule waliyekutana naye kabla ya tukio na ni tofauti na yule aliyekuwa anafanya tukio… ingawa ni kweli ndiye aliyesimama mbele yao wakati huo. Ajabu kweli.
Mwaka 1975, Milligan alifikishwa mahakamani na kuhumiwa kifungo jela kwa makosa ya ubakaji na ujambazi. Mwaka 1977 aliachiwa na kuwekwa kwenye kipindi cha matazamio. Hata hivyo, mwaka huohuo Milligan alikamatwa tena na kufikishwa mahakamani kwa kosa la kuwabaka wanawake watatu katika Chuo Kikuu cha Ohio.
Mhanga mmoja wa tukio hilo alifanikiwa kumtambua kwa kuangalia picha zilizowekwa kwenye orodha ya polisi ya wahalifu wa makosa ya kingono. Hata hivyo, mmoja kati ya wahanga wa matukio ya unyama na ubakaji wa Milligan alisema kuwa kabla ya tukio hilo, alimuona Milligan akiwa kama mtu mwema sana na wakati mwingine alikuwa kama mtoto mwenye umri wa miaka mitatu.
Polisi walimfungulia mashtaka matatu ya utekaji nyara, makosa matatu ya ujambazi na makosa manne ya ubakaji, na zaidi kuvunja masharti ya kipindi cha matazamio baada ya kutoka gerezani.
Wakati wa utetezi wake, wakili wake aliiambia Mahakama kuwa mteja wake (Milligan) alikuwa na matatizo ya utu ambayo kwake ni kama ulemavu na aliiomba Mahakama afanyiwe vipimo vya akili na saikolojia.
Mahakama ilikubali maombi hayo. Milligan alifanyiwa vipimo vya akili na saikolojia na Daktari Willis C. Driscoll. Mwingine aliyemfanyia vipimo zaidi ni mtaalam wa saikolojia, Dorothy Turner aliyefanya kazi katika kituo cha Southwest Community Mental Health Center, kilichoko Columbus, Ohio. Madaktari wote walibaini kuwa Milligan alikuwa na matatizo ya kisaikolojia yanayohusiana na utu asioweza kuudhibiti. Wakili anayemtetea akawasilisha utetezi wake mahakamani kwa kutumia vipimo hivyo, na mahakama ikaamua asiende jela bali awekwe chini ya uangalizi maalum akipata matibabu ya afya cha akili.
Baada ya kupata matibabu kwenye hospitali nyingi kubwa na vituo vya afya, mengi ya ajabu yalibainika. Ripoti kutoka katika Hospitali ya Anthen State ilibaini kuwa alikuwa na aina 10 za utu. Baadaye, aina nyingine 14 ambazo zilipewa jina la ‘Undesirables’ zilibainika na hizo zilikuwa hatari zaidi kwake. Hivyo, jumla ni kama watu 24 waliishi ndani ya Milligan, na mmoja tu ndiye alikuwa yeye halisi anayeweza kujiendesha kama wewe unavyoweza kuamua nini cha kufanya.
Madaktari waliofanya utafiti, walitoa majina kwa aina za utu au watu walioishi ndani ya Milligan kutokana na tabia zao. Kati yao ni pamoja na Arthur, huku alikuwa Muingereza aliyekuwa mtaalam wa sayansi na tiba; Allen, alikuwa na uwezo mkubwa wa kushawishi watu kwa uongo; Raen Vadascovinich, huyu alijionesha kama raia wa Yugoslavia ambaye Milligan alidai kuwa ndiye aliyefanya ujambazi kwa mtindo wa Robin Hood; na Adalana, huyu alikuwa msichana mwenye umri wa miaka 19 aliyekuwa na tabia za ushoga na usagaji, madaktari wanadai huyu ndiye alikuwa anawapikia wenzake chakula. Wengine walibainika kuwa walihusika kufanya ubakaji.
Ushahidi huo wa kidaktari na kitaalam zaidi ulipotua mahakamani, Mahakama ikaridhika nao na kumuondolea kabisa kifungo cha jela. Mwaka 1988 aliruhusiwa rasmi kutoka hospitali, na Agosti 1, 1991 Mahakama ilimuondolea vipindi vyote vya matazamio ili aishi kama mtu huru.
Alipambana na maisha na kuanzisha kampuni yake ya filamu aliyoiita Stormy Life Productions. Lakini kama ilivyo kwa watu wengi, alipata tatizo la mtaji, akashindwa kutimiza ndoto yake ya kuandaa filamu fupi.
Desemba 12, mwaka 2014, Milligan alifariki dunia kwa ugonjwa wa saratani akiwa na umri wa miaka 59.