Kamati ya Mamlaka ya Usalama nchini Urusi, imesema imeipata miili yote ya watu 10 katika eneo la ajali ya ndege inayodhaniwa kumuua Mkuu wa kundi la mamluki la Wagner, Yevgeny Prigozhin.
Kamati hiyo, inayochunguza ajali hiyo imesema katika taarifa yake kupitia mtandao wa Telegram kwamba imefanikiwa pia kuvipata vinasa sauti vinavyokuwapo ndani ya ndege ambavyo vitasaidia kujuwa uhalisia wa ajali.
Nchi kadhaa za Magharibi zimekuwa zikisema huenda Urusi ndiyo iliyohusika na ajali hiyo, kwa kuzingatia kwamba imetokea miezi miwili baada ya uasi wa muda mfupi wa Prigozhin, dhidi ya jeshi la Urusi.
Hata hivyo, Msemaji wa Ikulu ya Urusi ya Kremlin, Dmitry Peskov alikanusha vikali madai hayo akisema uvumi kuhusu ajali hiyo ni uongo huku shirika la ujasusi la Marekani likidai ndege hiyo ilidunguliwa na mlipuko wa kukusudia.