Mto mmoja amefariki na wengine sita kujeruhiwa katika ajali iliyotokea usiku wa kuamkia Septemba 4, 2023 katika eneo la Mataa ya Tumbaku lililopo Manispaa ya Morogoro Barabara kuu ya Morogoro kuelekea Iringa.
Ajali hiyo, imehusisha Lori la mizigo lenye namba za usajili T 862 DNH lililokua linatokea Dar es Salaam Kuelekea Iringa, kugongana na Basi la Abiria aina ya Tata, lenye namba za usajili T 994 DCH lililokua linatokea kituo cha Mabasi Mafiga Kuelekea Msamvu.
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na uokoaji Mkoani Morogoro amesema baada ya kufika katika tukio walifanya maokozi huku Majeruhi wakiwapatia huduma ya kwanza kabla ya kukimbizwa Hospitali na kwamba aliyefariki kwenye ajali hiyo ni Dereva wa Lori hilo na waliojeruhiwa ni abiria watano na dereva waliokuwepo kwenye basi la abiria.
Mashuhuda wa ajali hiyo wanasema walisikia mlio mkubwa mara tatu na waliposongelea eneo la tukio walikuta Dereva wa Lori amebanwa huku akivuja damu na wasafiri waliokuwa kwenye basi la abiria wakiwa na majeraha, huku chanzo cha ajali hiyo kikitajwa kuwa ni uzembe wa dereva wa Lori ambaye ni marehemu kuendesha kwa mwendokasi.