Rais Dkt. John Magufuli ametengua uteuzi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) Mhandisi Dkt. John Ndunguru na kuivunja bodi hiyo kuanzia leo Septemba 24, 2018.
Amechukua hatua hiyo kufuatia ajali ya kuzama kwa kivuko cha MV. Nyerere iliyotokea Septemba 20, 2018 na matukio mbalimbali ya ajali za barabarani hapa nchini yanayosababisha vifo, ulemavu na uharibifu wa mali.
Aidha, pamoja na hatua hiyo kamati ya uchunguzi ambayo itatangazwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa baadaye, itaendelea na uchunguzi wa ajali ya kivuko cha MV. Nyerere kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kama ilivyopangwa.
Pia utenguzi huo wa Rais Magufuli ni wa pili kuufanya tokea ilipotokea ajali ya kivuko cha Mv. Nyerere na kusababisha takribani ya watu 224 kufariki dunia kutokana na ajali hiyo.
Hata hivyo, Jana Septemba 23, 2018 Rais Magufuli aliivunja Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) iliyokuwa chini ya Brigedia Jenerali Mstaafu, Mabula Mashauri kufuatia kuzama kwa kivuko cha MV. Nyerere.