Mamlaka ya uokoaji nchini India imesema hawajafanikiwa kuwapata watu wengine walionusurika kwenye ajali iliyohusisha treni mbili za abiria na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 300.
Mkurugenzi wa kitengo cha dharura na zimamoto wa jimbo la Odisha, Sudhanshu Sarangi amesema walifanikiwa kuwaokoa watu walionusurika na baada ya hapo shughuli iliyofuata ilikuwa ya kuitoa miili ya watu waliokufa kwenye ajali.
Mamia ya watu walijeruhiwa kufuatia ajali hiyo mbaya zaidi kuwahi kutokea kwa miongo kadhaa, ikihusisha Treni ya Coromandel Express iliyokuwa ikisafiri kutoka Howrah, jimbo la Bengali magharibi kuelekea Chena, jimboni Tamil Nadu, na Howrah Superfast Express iliyokuwa ikisafiri kutoka Bengaluru huko Karnataka kuelekea Howrah.
Tayari Waziri Mkuu wa India, Narendra Mordi amekutana na maafisa mjini New Delhi na kuelezea kushtushwa na ajali hiyo na baadaye alisafiri kuelekea Odisha kwa lengo la kutembelea eneo la tukio na kufika kwenye hospitali wanakotibiwa majeruhi.