Viongozi wa mataifa ya Kusini mwa Afrika wamekutana jijini Kinshasa kwa mkutano wao wa 42, ambapo wamejadili hatua iliyofikiwa katika utangamano wa karibu na kuimarisha biashara ya kikanda.
Mkutano huo umefanyika chini ya kauli mbiu isemayo, Kukuza Ukuaji wa Viwanda kupitia Sekta ya Kilimo, Urutubishaji wa Rasilimali za Madini na Minyororo ya Thamani ya Kikanda kwa Ukuaji wa Uchumi Shirikishi na Ustahimilivu.
Mkutano huo unakuja wakati nchi mwenyeji (DRC), inakabiliwa na ghasia mpya eneo la mashariki huku Rais, Felix Tshisekedi akishutumu ‘uchokozi wa kinyama unaoleta madhara’ dhidi ya nchi yake unaofanywa na nchi ya Rwanda.
Baadhi ya nchi wanachama wa SADC kama ikiwemo Tanzania iliyoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan na wajumbe kutoka Malawi, wamekuwa ni wachangiaji wa askari katika Kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa chini ya MONUSCO.
Mwanachama mwingine wa umoja huo ni Msumbiji, ambayo pia inakabiliana na waasi wa wanamgambo katika majimbo yake ya kaskazini huku kikosi cha kikanda kinachojulikana kama SAMIM, pamoja na vikosi vya Rwanda vikifanikiwa kushinda eneo la waasi wanaohusishwa na Islamic State.
Mwishoni mwa mkutano huo, Kongo itachukua nafasi ya urais wa zamu wa umoja huo kutoka Malawi ambapo Mtanzania Brigedia Jenerali Juma Nkangaa Sipe akiwa Mkurugenzi wa asasi ya siasa, ulinzi na usalama katika sekretarieti ya SADC.