Serikali imesema itaajiri walimu wapya 6,000 wa Shule za Msingi na Sekondari ifikapo Juni 2021, ili kujaza nafasi zilizoachwa na walimu waliofariki au kustaafu kazi.
Ahadi hiyo imetolewa leo Ijumaa Aprili 9, 2021 na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) David Silinde wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Njombe Mjini (CCM), Deodatus Mwanyika.
Mbunge huyo amehoji Serikali inachukua hatua gani kumaliza tatizo la upungufu wa Walimu nchini hasa Shule zilizopo maeneo ya Vijijini.
Akijibu swali hilo Silinde amesema Ofisi ya TAMISEMI kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora) na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia itaajiri walimu wapya 6,000 wa Shule za Msingi na Sekondari ifikapo Juni mwaka huu ili kujaza nafasi zilizoachwa na walimu waliofariki ama kustaafu kazi.
Amesema Tamisemi imekuwa ikifanya uhamisho wa ndani kwa kuwahamisha walimu waliozidi hasa kwenye maeneo ya mijini na kuwapanga kwenye shule zenye uhaba mkubwa wa walimu hasa zilizopo maeneo ya vijijini.
“Serikali itaendelea kuajiri na kuwapanga walimu kwenye shule za msingi na sekondari hasa zenye mahitaji makubwa kwa kadri ya upatikanaji wa fedha,”amesema.