Mamlaka ya Dawa, Vifaa Tiba na Vitendanishi (TMDA), Nyanda za Juu Kusini, kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, imekamata shehena ya dawa zenye thamani ya shilingi millioni 7.7 zilizokwisha muda wake katika nyumba ya mkazi mmoja wa Igawilo jijini Mbeya.
Kaimu Meneja wa TMDA, Nyanda za Juu Kusini, Anitha Mshighati amesema walipata taarifa kutoka kwa wasamaria wema kuwepo kwa mtu huyo ambaye amepakia shehena ya dawa, vifaa tiba na vitendanishi katika nyumba yake huku akiendelea kuuza licha ya muda wake kuisha, akitumia mihuri na vifaa vingine kubadilisha ili zionekane hazijaisha muda wake.
Dawa na vifaa tiba vilibvyokamatwa ni pamoja na antibayotiki, sindano na nyuzi za kushonea, malaria na asidi ambazo ni za serikali zikiwa zimefutwa lebo.
“Dawa zote zimekutwa katika makazi ya mtu zikiwa zimewekwa katika hali isiyofaa bila mpangilio wowote kinyume cha sheria ya dawa ya vifaa tiba na sheria ya nchi sura ya 219 ya mwaka 2013 kwa sababu vitu vilivyokutwa ni mali ya serikali, tumeorodhesha dawa zote na zimechukuliwa, mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kwa ajili ya utaratibu mwingine,” Amesema Mshighati.
Aidha, TMDA inaendelea kudhibiti mpaka wa Tunduma na Kasumulu ili dawa za magendo na zilizokwisha muda wake zisiingizwe nchini huku wakiendelea kutoa elimu kwa wananchi kuepukana na athari za kiafya.