Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam leo imeridhia maombi na hoja za wabunge 19 wa viti maalum waliokuwa wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ya kukipinga kuvuliwa uachama wa chama hicho.
Ikitoa aamuzi wa maombi ya wabunge hao wanaoongozwa na Halima Mdee yaliyosikilizwa Juni 30, 2022 na Jaji Mustapha Ismail, Mahakama Kuu imewaruhusu kufungua shauri hilo dhidi ya CHADEMA, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Katika maombi yao, pamoja na mambo mengine Mdee na wenzake wanaiomba Mahakama kufanya mapitio ya kimahakama ya mchakato wa kuvuliwa uanachama wao.
Wanasiasa hao 19 waliongozwa na jopo la mawakili lilioundwa na Aliko Mwamanenge, Ipilinga Panya, Edson Kilatu na Emmanuel Ukashu. Jopo la mawakili wa Chadema linaongozwa na Peter Kibatala.