Utanielewa kwanini ninaiita hii ‘dunia ya mitandaoni’… Kama hauishi huko hautaona kama kuna maana, lakini wakaazi wa huko hasa katika mtaa na kijiji cha ‘udaku’, wanahudhuria vikao vya dharura vya kushuhudia migororo na vita kuu zisizoisha, vituko na shangwe pia.
Sasa ule ugomvi wa Mange Kimambi na mrembo kutoka Uganda, Zari The Boss Lady ameununua Mwimbaji kutoka Kenya, Akothee na hivyo kutanua wigo wa kinachoendelea kati ya Malkia hao wawili wa Instagram kwani hivi sasa mashabiki kutoka Kenya nao ‘wako rada’.
Ni kama Akothee, mwimbaji wa kike mwenye utajiri mkubwa amekuja kuunganisha nguvu ya Zari dhidi ya Mange baada ya kukerwa na jinsi ambavyo amekuwa akimshambulia kwenye Instagram.
Akothee amerekodi kipande cha video akitoa ushauri na kulaani vikali maisha ya Mange mitandaoni dhidi ya watu wengine, akitaja vijembe vya Mange kuhusu nyumba anayokaa Zari nchini Afrika Kusini kuwa ni ya Diamond. Amemtaka aachane na maisha ya watu, apambane na hali yake.
Mange amekuwa akitembelea kauli ya Diamond ambaye ni baba wa watoto wawili wa Zari aliyoitoa hivi karibuni kupitia Wasafi FM kuwa ana uwezo wa kumuondoa mzazi mwenzake kwenye nyumba yake ya Afrika Kusini kwani anazo nyaraka zote, ila amemheshimu kwakuwa anakaa na wanaye. Hivyo, Mange amekuwa akihoji kama Zari ni tajiri kama anavyodai kwanini akubali kudhalilishwa kwa nyumba anayoishi.
Akothee amekuja kama dada mkubwa na kumpa makavu Mange:
“Kuna watu wanajua maisha ya watu wengine kama nyuma ya mikono yao kwenye mitandao ya kijamii. Watu haohao hawana maisha nje ya mitandao ya kijamii. ‘Ooh, hiyo nyumba sio yake, ooh ataishiwa hivi karibuni,
“Asilimia 60 ya mambo unayozungumza kwenye mitandao ni kuhusu maisha ya watu wengine, ni muda gani unaotumia kujikita kwenye mambo yako? Ni muda gani unachangia kwenye maisha yako mwenyewe? Na hata kama nyumba sio ya kwao, Je, wanaishi nyumbani kwako? Wanakuomba kodi? Wamewahi kugonga mlango wako? Ukijiuliza maswali haya yote utagundua kuwa wewe ni mjinga mwenye kipaji,
“Achana na watu kwenye mitandao ya kijamii, watu wanakuja kwenye mitandao ya kijamii kufurahi na sio kurushiana maneno ya chuki kulia na kushoto. Hii inatuonesha wewe ni mtu wa aina gani.. wewe ni kahaba mwenye chuki uliyefulia, kwa sababu watu matajiri hawatukani watu kwenye mitandao bali wao hupost mambo yao na kuondoka. Kwahiyo ni kazi kwenu nyie mliofulia kuchunguza ‘ooh sio yake, anajinunulia mwenyewe, wataachana hivi karibuni… wajinga, nawaita wajinga! Tafuta maisha yako, jikite kwenye maisha yako na achana na watu. Kama wanacho au hawana haitakusaidia wewe.”