Baada ya kiungo Mnigeria Victor Akpan na beki Mburkina Faso Mohamed Ouattara kukosa nafasi ya kucheza mara kwa mara kwenye kikosi cha Simba, kocha mkuu wa timu hiyo, Juma Mgunda amevunja ukimya na kueleza kuwa kwenye mipango ya kuanza kuwapa nafasi.
Wachezaji hao walisajiliwa na timu hiyo, mwanzoni mwa msimu huu, Ouattara akitokea Al Hilal ya Sudan huku Akpan akinunuliwa kutoka Coastal Union lakini tangu watue Msimbazi hawajawa na mwenendo mzuri kama walivyotarajiwa.
Mgunda ameeleza sababu ya kutomwona Akpan uwanjani akicheza ni kutokana na kuumia siku chache baada ya kujiunga na Simba ila sasa amepona.
“Akpan ni mchezaji mzuri, ni kijana wangu tangu tupo Coastal Union na alifanya vizuri. Kilichotokea mwanzoni mwa msimu huu alipata majeraha ya goti na kumlazimu kukaa nje, kwa sasa amepona lakini siwezi kumwingiza moja kwa moja mchezoni kwani anahitaji kupona taratibu,” alisema Mgunda.
Kwa upande wa Ouattara, Mgunda alieleza ubora na mawasiliano ya Henoc Inonga na Joash Onyango wanaouonyesha kwa sasa ni ngumu kuwapangua lakini alisema atacheza tu kwani kuna mbinu na mifumo tofauti inayomhitaji.
“Sio Ouattara tu, hata Kennedy Juma naye hajapata muda wa kutosha kucheza kutokana na wanaocheza kuwa na maelewano zaidi.
Haipaswi kuwalinganisha au kuwagombanisha kwani kila mchezaji aliyesajiliwa Simba yupo hapa kuhakikisha malengo ya timu yanatimia na wote watacheza,” alisema Mgunda
Hata hivyo, ilielezwa kutokana na kutopata nafasi hiyo, Ouattara ataachana na timu hiyo wakati wa dirisha dogo la usajili la Desemba.
Sambamba na Ouattara na Akpan, wachezaji wengine wa Simba ambao hawapati nafasi ya kucheza mara kwa mara ndani ya kikosi hicho ni Peter Banda, Gadiel Michael, Nelson Okwa na John Bocco.