Mabingwa wa Soka Barani Afrika Al Ahly, wamerejea katika harakati za kutaka kumsajili Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Msumbiji na Klabu Bingwa Tanzania Bara Simba SC Luis Miquissone.
Kwa mujibu wa Tovuti ya Youm ya nchini Misri, Mabingwa hao wa Afrika wanatajwa kufanya mawasiliano ya awali na Uongozi wa Simba SC, ili kuangalia uwezekano wa kumsajili Miquissone.
Mtandao huo umefafanua kuwa, Miquissone ni miongoni mwa wachezaji watatu ambao klabu hiyo imejipanga kuwasajili kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu ya Misri na Michuano ya Kimataifa.
Wachezaji wengine wawili waliotajwa na Tovuti hiyo ni Soufiane Rahimi wa Raja Casablanca ya Morocco na Gaston Sirino wa Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.
Miquissone aliwavutia Al Ahly baada ya kuonesha kiwango cha hali ya juu kwenye michuano ya Klabu Bingwa Barani Afrika hatua ya makundi msimu wa 2020-21.
Kiungo huyo ndiye aliwafunga Al Ahly katika mchezo wa mzunguuko wa pili hatua ya Makundi, Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.