Wapinzani wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans kwenye Michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika Al Hilal ya Sudan, wanatarajiwa kuwasili jijini Dar es salaam leo Alhamis (Oktoba 06) majira ya kumi na mbili jioni.
Young Africans itakua mwenyeji wa mchezo wa Mkondo wa Kwanza utakaopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam Jumamosi (Oktoba 08) saa kumi jioni, huku ikitarajia kwenda Sudan kwa mchezo wa Mkondo wa Pili utakaopigwa mwishoni mwa juma lijalo katika Dimba na Al Hilal mjini Khartoum.
Akizungumza na Dar24 Media Afisa wa Al Hilal aliyetangulia Dar es salaam kwa ajili ya kuweka mambo sawa kabla ya kuwasili kwa kikosi chao, amesema msafara wachezaji 23, Benchi la Ufundi la watu 8 na viongozi 7, wataanza safari ya kutoka Lumbumbashi kuja Dar es salaam leo majira ya saa nane mchana
Amesema maandalizi ya kupokewa kwa kikosi chao kitakapowasili jijini Dar es salaam yamekamilika na kikosi kitakapowasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Waandishi wa Habari watapata nafasi ya kuzungumza na Mkuu wa Msafara.
“Maandalizi ya kuwapokea watu wetu yameshakamilika, nimekua hapo kwa siku kadhaa kukamilisha mpango wa maandalizi ya kuelekea mchezo wetu dhidi ya Young Africans, Kikosi na Benchi la Ufundi kitawasili hapa saa kumi na mbili jioni.”
“Tunatarajia kuwa na mchezo mzuri dhidi ya Young Africans, tunachosisitiza tunahitaji mchezo wa kiungwana iwe ndani ama nje ya Uwanja, soka ni mchezo wa urafiki, sio uadui.” amesema Afisa huyo
Al Hilal wanatokea DR Congo walipoweka kambi ya siku 6 kwa kucheza michezo miwili ya kirafiki dhidi ya Don Bosco na AS Vita Club, ikiwa ni sehemu ya maandalizi yao kuelekea mchezo dhidi ya Young Africans.