Wakati Kikosi cha Al Hilal kikitarajiwa kuwasili saa kumi na mbili jioni kikitokea DR Congo, Msafara wa Klabu hiyo umekamilisha zoezi la vipimo vya Covid-19 jijini Lubumbashi kabla ya kuanza safari ya kuja Tanzania.

Al Hilal itacheza dhidi ya Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Mkondo wa Kwanza Jumamosi (Oktoba 08), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Msafara huo wa Al Hilal uliosheheni wachezaji 23, Benchi la Ufundi la watu 8 na Viongozi 7 wa AL Hilal ya Sudan, ulifanya vipimo vya Covid-19, jana Jumatano (Oktoba 05), mjini Lubumbashi ili kuepuka usumbufu ambao wanahisi huenda ukajitokeza watakapowasili Dar es salaam.

Al Hilal waliweka Kambi ya siku sita mjini Lubumbashi-DR Congo na kucheza michezo miwili ya kirafiki dhidi ya Don Bosco na AS Vita Club, ikiwa ni sehemu ya maandalizi yao kuelekea mchezo dhidi ya Young Africans.

Wakati huo huo Mkurugenzi wa Mashindano wa Young Africans Saad Kawembwa amesema Uongozi umeshafanya maandalizi yote kwa ajili ya kuwapokea wageni hao kutoka Sudan.

“Kila kitu kinakwenda vizuri mpaka sasa. Na jambo zuri ni kwamba tuna mawasiliano mazuri na wenzetu mpaka sasa. Kama Klabu tumejiandaa kuwapokea na tutawapa ushirikiano mzuri wakati wote watakapokuwa Tanzania,” alisema Kawembwa

Mchezo wa Young Africans dhidi ya Al Hilal umepangwa kuanza majira ya 10:00 jioni, Jumamosi (Oktoba 08), Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es salaam.

TAWA mwenyeji mjadala wa Kimataifa utalii barani Afrika
Saudi Arabia, Urusi zaazimia 'kuikomoa' Marekani