Klabu ya Azam FC huenda ikashindwa kufikia ndoto za kumuajiri Kocha kutoka DR Congo Florent Ibenge ambaye anatajwa kuwaniwa miamba hiyo ya Azam Complex mwishoni mwa msimu huu 2022/23.

Azam FC kwa sasa inatafuta kocha mpya ambaye atapata nafasi ya kukisoma kikosi kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa Ligi Kuu na Michuano ya Kimataifa.

Taarifa kutoka Sudan zinaeleza kuwa Mabosi wa klabu ya Al Hilal ambayo ina mkataba wa Ibenge, wametibua dili la Azam FC baada ya kumwekea kocha huyo fedha za maana mezani ili kusalia Omdurman.

Klabu ya Azam FC inadaiwa kufanya mazungumzo na Ibenge na kumpa ofa ya kutua Dar es Salaam kuchukua mikoba iliyoachwa na Mfaransa Denis Lavagne, lakini hakujibu ofa hiyo licha ya mawasiliano ya kawaida baina yake na mabosi wa klabu hiyo wanaoamini kocha huyo anaweza kuibadili timu hiyo na kuipa mafanikio kama alivyofanya kwa Al Hilal.

Hata hivyo, huenda dili hilo likaota mbawa kama Ibenge atafanikiwa kuifikisha Al Hilal Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa ambapo anahitajika kushinda au kutoa sare mchezo wa mwisho dhidi ya Al Ahly ya Misri ugenini ambapo matajiri wa Hilal wamemuahidi kumuongezea maslahi mara mbili ya anachokipata sasa, pesa ambayo ni nyingi sana kwa Azam FC.

Pamoja na sekeseke hilo, taarifa kutoka Azam FC zimeeleza bado hawajakata tamaa ya kumpata Ibenge lakini hata ikitokea wakamkosa bali watashusha kocha mwingine mwenye uzoefu na soka la Afrika kutoka mataifa ya Ulaya.

“Wale jamaa (Hilal) wamemuahidi Ibeng pesa nyingi kama atatinga robo fainali pia bado wana mpango naye wa muda mrefu,” kilieleza chanzo na kuongeza: “Lakini bado hatujaka tamaa, tunawasiliana naye na kumshawishi na kama tutaona haiwezekani kabisa tutaleta kocha mwingine ambaye yupo kwenye Top Four (nne bora) ya listi yetu na huyo atatoka Ulaya ila analijua vyema soka la ukanda huu.”

Agizo la Rais huwa halipingwi: Waziri Mkuu
Kocha Taifa Stars: Uganda ni wagumu