Klabu ya Al Merrikh ya Sudan imetangaza kuwa watacheza michezo yao ya nyumbani ya Hatua ya Makundi Ligi ya Mabingwa Barani Afrika katika uwanja wa Al Hilal.

Hii ni kutokana na uwanja wao wa Al Merrikh, kushindwa kukidhi Viwango vya uwanja vya Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’.

Akitangaza uamuzi wa kutumia uwanja huo, Mkurugenzi Mkuu wa Al Merrikh, Haitham Mohamed amesema: “Baada ya kufikia makubaliano na klabu ya Al Hilal kutumia Uwanja wa Al Hilal, klabu yetu itazingatia kanuni zote za uwekezaji na utunzaji wa Uwanja huo.”

“Tunawaomba Mashabiki wote wa Al Merrikh kusimama nyuma ya timu katika kipindi kijacho ili kupata matokeo yanayotarajiwa na yatakayotupatia nafasi ya kutinga Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika,” Mohamed aliongeza.

Uwanja wa Al Hilal upo Omdurman Jimbo la Khartoum nchini Sudan, ni uwanja rasmi wa nyumbani wa klabu ya Al-Hilal Club wenye uwezo wa kuchukua Mashabiki 65,000 walioketi.

Al Merrikh imepangwa katika Kundi D lenye timu za Zamalek (Misri), Espérance de Tunis (Tunisia), na CR Belouizdad (Algeria) na mchezo wao wa kwanza nyumbani wataivaa na Zamalek February 17, 2023.

Ofisi ya RC Katavi yatoa zawadi ya Christmas kwa watoto yatima
Ibrahim Ajibu: Sijaondoka Azam FC kwa kushuka kiwango