Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi, kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan imekabidhi zawadi mbalimbali kwa kituo cha kulelea watoto na wanaoishi katika mazingira magumu cha Mtakatifu Yohana Paul II (matumaini mapya ya watoto) kilichopo Nsemlwa mjini Mpanda.

Zawadi hizo zilizokabidhiwa kituoni hapo hii leo Desemba 23, 2022 ni mbuzi wawili, mchele kg 50, maharage kg 50, mafuta ya kula lita 20, juisi na pipi kwa ajili ya watoto hao wanaopokelewa kituoni hapo, ambao waliopitia unyanyasaji na ukatili wa kijinsia, waliotelekezwa na waliofiwa na wazazi wao.

Mkuu wa wilaya ya Mpanda Jamila Yusuf (wa pili kushoto), akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko kukabidhi zawadi ya sikukuu kwa watoto hao.

Akikabidhi zawadi hiyo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi, mkuu wa wilaya ya Mpanda Jamila Yusuf, amesema zawadi hizo ni katika mpango wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuwafariji na kuhakikisha makundi yote yanasherehekea vema sikukuu ya Christmas.

Msimamizi wa kituo hicho Sister Rose Sungura amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuyakumbuka makundi ya aina hiyo na kutoa wito kwa taasisi mbalimbali na watu binafsi kuwa na moyo wa kuwasaidia wasiojiweza ili na wao washerehekee kwa usawa msimu huu wa sikukuu.

Kituo hicho kilianzishwa mwaka 2016 na kuanza kazi mwaka 2019 kikiwa na watoto 57 ambapo kati ya hao 5 walitangulia mbele ya haki, 30 wamekabidhiwa kwa ndugu zao na 22 wamesalia kituoni.

Moses Phiri njia panda kuivaa KMC FC
Al Merreikh kufuata kanuni Al-Hilal Stadium