Kundi la kigaidi la Al-Shabaab imewateka madaktari bingwa wawili kutoka Cuba katika mji wa Mandera nchini Kenya.
Kwa mujibu Citizen, magaidi hao waliteka gari lililokuwa na madaktari hao na kumuua mmoja kati ya walinzi wao binafsi (bodyguards) na kisha kutokomea nao kusikojulikana.
Msemaji wa Polisi, Charles Owino amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa vyombo vya usalama vinaendelea kulifanyia kazi ikiwa ni pamoja na kuwatafuta madaktari hao.
“Walitekwa wakiwa wanaelekea kazini na gari walilokuwa nalo tumelipata. Tunamshikilia dereva na tunaendelea kumhoji,” Owino alisema jana, Aprili 11, 2019.
Shuhuda wa tukio hilo ameeleza kuwa aliwaona wapiganaji wa Al-Shabaab wakivuka kuelekea Somalia wakiwa na madaktari hao.
Madaktari hao ni miongoni mwa watalaam wa tiba 100 kutoka nchini Cuba waliowasili nchini Kenya Juni 2018.
Wapiganaji wa Al-Shabaab wamekuwa wakiiandama Kenya wakipinga hatua ya nchi hiyo kupeleka vikosi vyake nchini Somalia kuisaidia Serikali kupambana nao.