Kiongozi wa upinzani wa Urusi, Alexei Navalny, ameruhusiwa kutoka hospitali baada ya kulazwa kwa siku 32 katika hospitali ya Charite mjini Berlin nchini Ujerumani iliyokuwa ikimhudumia.
Uongozi wa hospitali hiyo umesema kwa kuzingatia maendeleo ya mgonjwa katika matibabu na hali yake ya sasa wanaamini inawezekana akapona kabisa ingawa ni mapema mno kutathmini athari za muda mrefu za sumu aliyotiliwa.
Wataalamu wa silaha za sumu wa Ujerumani wamebaini kuwa mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 44 alitiliwa sumu ya mishipa ya enzi ya zamani ya muungano wa Sovieti.
Ugunduzi huo uliifanya serikali ya Ujerumani mjini Berlin kuitaka Urusi ichunguze kisa hicho.
Timu ya Navalny waliutuhumu utawala wa Kremlin kwa kuhusika kumtilia sumu kiongozi huyo wa upinzani, lakini maafisa wa Urusi wameyapinga vikali madai hayo.
Utawala wa Kremlin umepuuzilia mbali miito ya kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, na viongozi wengine kujibu maswali kuhusu kutiliwa sumu aina ya Novichok kiongozi huyo.