Kiungo kutoka nchini Argentina ambaye alikuwa sehemu ya Kikosi kilichotwaa ubingwa wa Kombe la Duinia 2022 Alexis Mac Allister, amesema bado ni mwenye furaha katika Klabu ya Brighton and Holve Albion na hana haraka ya kuondoka.
Kiungo huyo aliyeng’ara vilivyo katika Fainali za Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar, anahusishwa na taarifa kadhaa za kuihama klabu hiyo wakati wa Dirisha Dogo la Usajili 2023, huku klabu za Arsenal na Tottenham zote za jijini London zikitajwa kuiwania saini yake.
Mac Allister mwenye umri wa miaka 24, alitoa kauli ya kuwa na furaha baada ya kurejea Brighton and Holve Albion akitokea nchini kwao Argentina jana Jumatatu (Januari 02), na kupata mapokezi ya heshima kutoka kwa viongozi na Wachezaji wenzake.
“Ninajihisi furaha kubwa kuwa hapa, nina amani kubwa ya kuendelea kucheza Brighton and Holve Albion, sina haraka ya kuondoka,”
“Nitajitahidi kucheza kwa bidii zaidi ili kuisaidia klabu kufikia malengo yake mwishoni mwa msimu huu, ninaamini kuna kitu nitakiongeza kwenye timu nitakaporejea kwenye kikosi, nipo tayari kwa lolote kwa ajili ya klabu hii.”
Mac Allister alisajiliwa Brighton Januari 2019 na mwezi Oktoba 2022 alisaini mkataba mpya ambao unaendelea kumuweka Klabuni hapo hadi mwaka 2025.