Kiungo Feisal Salum Abdallah (Feitoto) ameendelea kuzua mijadala kwa wadau wa mchezo wa soka nchini baada ya kuonekana akiwa katika ardhi ya Falme za Kiarabu akifanya mazoezi kwenye moja ya Kituo ambacho hakijafahamika jina lake kwa haraka.

Feitoto amechapisha baadhi ya picha akifanya mazoezi hayo kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii ikiwa ni siku kadhaa tangu kudaiwa kuvunja mkataba na Yanga SC na kuondoka kwenye kambi ya timu hiyo iliyopo Avic Town,Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Kupitia chapisho lake katika mtandao wa Twitter, Feisal ameandika: “Haina kufeli, hakuna kukata tamaa tuzidi kuzikimbilia ndoto zetu, Mwaka Mpya.”

Ujumbe huo unaweza kuwa ni ishara ya Kiungo huyo kutoka visiwani Zanzibar kuamua kubadilisha mazingira na kuchagua kucheza soka nje ya mipaka ya Tanzania.

Hata hivyo, Feisal huenda labda akasajiliwa na moja ya timu za Falme za Kiarabu kutokana na kiwango chake bora alichokionyesha muda wote akiwa na Mabingwa wa Tanzania Bara Young Africans.

Feisal alidumu katika Kikosi cha Wananchi akicheza nafasi ya Kiungo hususani Kiungo cha Ushambuliaji na mara nyingi amehusika kwenye upachikaji wa mabao katika Klabu hiyo.

Desemba 24, 2022 Feisal alichapisha ujumbe kwenye ukurasa zake za mitandao ya kijamii akiwaaga Wananchi baada ya kudaiwa kuvunja mkataba wake na timu hiyo, licha ya Wananchi wenyewe kudai kuwa Kiungo huyo ana mkataba Klabuni hapo hadi ifikapo mwaka 2024.

Shule kutofunguliwa kutokana na kipindupindu
Alexis Mac Allister azikataa Arsenal, Spurs