Dori Joshua, mkaazi wa kijiji cha Endakiso wilaya ya Babati Mkoani Manyara amekamatwa kwa kosa la kuiba mtoto aliyekuwa na umri wa siku moja.
Kamanda wa polisi mkoa wa Manyara, Augustine Senga amewaambia waandishi wa habari kuwa Dori mwenye umri wa miaka 20, alimchukua mtoto huyo kutoka kwa mama yake aliyekuwa amepanda naye bajaji na kisha kutokomea naye. Tukio hilo lilitokea wiki iliyopita.
Kamanda Senga ameeleza kuwa Dori alimshawishi mama wa mtoto huyo, Hawa Msangi aliyekuwa anatoka katika hospitali ya Wilaya ya Babati (Mrara) wachukue bajaji moja ili kupunguza gharama, zoezi ambalo alifanikiwa.
Ameeleza kuwa wakiwa kwenye bajaji hiyo, Dori alimuomba mama huyo ambebe mwanaye ili kumsaidia, lakini walipofika katika eneo la Sinai, alimuomba dereva asimame ili ashuke mara moja achukue pesa kwa ndugu yake ili waendelee na safari. Na alifanikiwa kushuka akiwa amembeba mtoto huyo, lakini ghafla alitokomea naye.
Baada ya Polisi kupata ripoti, walifuatilia kwa haraka tukio hilo na kuambiwa kuwa mwanamke huyo aliondoka katika eneo hilo kwa usafiri wa bodaboda kuelekea katika kijiji cha Endakiso.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi, walifanikiwa kufika nyumbani kwao na kumkuta akiwa nje ya nyumba huku mtoto akiwa amelazwa kwenye moja ya vyumba vya nyumba yao; hivyo walimrejesha mtoto huyo kwa mama yake.
Amesema baada ya kumhoji, Dori alidai kuwa alitaka amuoneshe mchumba wake ambaye alikuwa amemdanganya kwa miezi kadhaa kuwa ana ujauzito, ili aweze kumpa pesa.
Kamanda Senga aliwataka wanawake kuwa makini baada ya kujifungua kwani wapo watu waovu wanaopanga kuiba watoto. Pia, aliwataka watu wenye tabia hiyo kuacha mara moja kwani mkono wa sheria hautawaacha salama.