Rais wa kwanza wa Zambia, Kenneth Kaunda amefariki dunia leo Juni 17, 2021 akiwa na umri wa miaka 97.
Siku chache zilizopita, Kenneth David Kaunda anayefahamika zaidi kama KK alilazwa katika Hospitali ya Maina Soko jijini Lusaka kufuatia maradhi yaliyokuwa yanamsumbua kwa siku kadhaa.
Ingawa taarifa kutoka ofisi ya Rais haikueleza ni nini haswa alichokuwa anaumwa, vyombo mbalimbali vya habari nchini humo viliripoti kuwa alikuwa akisumbuliwa na homa ya mapafu aina ya (Pneumonia).
Kaunda aliyezaliwa April 28, 1924, aliiongoza Zambia kuanzia Oktoba 24, 1964 wakati Taifa hilo la kusini mwa Afrika lilipojipatia uhuru hadi Novemba 2, 1991 na alikuwa miongoni mwa mashujaa wachache walioshiriki kuikomboa Afrika.
Kaunda alikuwa kiongozi wa chama cha United National Independence Party (UNIP), pia alipewa jina la utani Gandhi wa Afrika kutokana na harakati zake za kupigania uhuru katika miaka ya 1960 .
Wakati akiwa madarakani aliongoza harakati nyingi za kupigania uhuru na usawa wa watu weusi katika bara la Afrika ikiwa ni pamoja na kuongoza kongamano la Taifa la Afrika Kusini (ANC).
Baadaye alirudi tena katika siasa akisaidia kupambana na migogoro katika nchini ya Zimbabwe pamoja na Kenya.
Kaunda pia alikuwa mwanaharakati wa mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi na aliwahi kutangaza hadharani kuwa mwanaye amefariki na ugonjwa huo.
Watu mashuhuri mbalimbali wameanza kutuma salamu zao za pole akiwemo Rais wa Zambia, Edgar Lungu ambaye kupitia ukurasa wake wa Twittwe ameandika, ” Mpendwa KK, Ni kwa huzuni kubwa nimepokea taarifa juu ya kifo chako. Umeondoka katika wakati ambao hatukutarajia lakini tunafarijika kwamba sasa uko na Baba Yetu, Mungu Mwenyezi mbinguni.
Ninaiombea familia ya Kaunda ifarijike tunapoomboleza kifo cha shujaa wa wa kweli wa Kiafrika.”
Naye Mchezaji wa zamani wa kimataifa kutokea nchini Zambia, kalusha bwalya ameandika katika ukurasa wake wa twitter, “Kwaheri kwako Rais Kenneth Kaunda. Ninajivunia na siku zote nitajivunia kuwa mwanachama wa “KK11”. Utu na heshima. Roho yako ipumzike kwa Amani Milele, ukijua matokeo makubwa uliyotutolea sisi wote Wazambia, Waafrika na Ulimwengu kwa ujumla. Salamu za pole kwa familia.”