Polisi aliyehusika na kifo cha Suguta Chacha ambaye ni mdogo wa Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche na kumsababishia kifo ametiwa hatiani na kupandishwa kizimbani na kusomewa shitaka la mauaji.
Kufuatia hatua hiyo Familia ya Marehemu imesema baada ya kufanya mashauriano ya muda mrefu familia imekubali kumzika ndugu yao ambapo mazishi yatafanyika Alhamisi ya Mei 3, 2018 kijiji cha Nyabitocho mara baada ya familia kuridhika hatua zilizochukuliwa dhidi ya mtuhumiwa.
Hayo yamesemwa na Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche ambaye ndiye msemaji wa familia na kaka wa marehemu.
Hivyo familia imekubali kuchukua mwili huo na tayari kwa kuuzika, Heche alitumia kurasa zake za mitandao ya kijamii kutoa taarifa hiyo kwa umma.
”Tumeridhika na hatua zilizochukuliwa na jeshi la polisi kwa kumtia hatiani mtuhumiwa kumfikisha mahakamani na kusomewa shtaka la kuua, kama familia tumeona ni vyema tuutangazie umma kuwa kesho tutauchukua mwili wa marehemu na kuuleta nyumbani na kesho kutwa (Alhamisi Mei 3) tutamzika” amesema Heche.
Aidha ametoa shukrani kwa Watanzania na wananchi wa Tarime kwa jinsi ambavyo wamepaza sauti kukemea mauaji ya kinyama na hatimaye mtuhumiwa amepandishwa kizimbani.
Ameongezea kwa kuwaomba watanzania kuendelea kukemea matendo na matukio haya ya kinyama ili yasimpate Mtanzania mwingine.